9/24/2010

Mkutano wa Kampeni Loliondo: JK aahidi kupunguza tatizo la maji Wilayani Ngorongoro

 Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Kikwete akimpa mkono mtoto mdogo aliyefika katika uwanja wa ndege wa Loliondo na baba yake kwa ajili ya kumpokea huku mtoto mwingine naye akijitahidi kunyosha mkono wake ili naye
 amsalimie Rais Kikwete

 Rais Jakaya Kikwete ambaye ni mgombea Urais kupitia CCM akinadi sera zake kwa wananchi wa mji wa Loliondo ambao ni makao makuu ya wilaya ya Ngorongoro katika mkoa wa Arusha


Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kwa miaka mitano ijayo, serikali imenuia kumaliza tatizo la maji Ngorongoro.

Akihutubia wananchi wa Loliondo wilayani hapo, Mheshimiwa Kikwete alisema vijiji vya Malambo, Masusu, Digodigo, na vingine saba vimeanza kuhudumiwa ili kuhakikisha wananchi wa huko wanapata maji safi na salama. Mradi huu wa kuhudumia vijiji kumi kila Mkoa unafadhiliwa na Benki ya dunia.

Mipango mingine ya CCM kwa miaka mitano ijayo ni katika usambazaji wa umeme Mji wa Loliondo na ujenzi wa barabara.

Mheshimiwa Kikwete alisema miaka mitano iliyopita, CCM iliahidi kuongeza pesa kwenye mfuko wa barabara. Hivi sasa halmashauri ya mji wa Loliondo imeshapewa bilioni mbili kwa ajili ya kuboresha barabara za halmashauri.

Akizungumzia upotoshwaji wa ujenzi ya barabara ya lami  kwenye hifadhi ya Serengeti, Mheshimiwa kikwete alisema yeye anaamini kuwa kujenga barabara ya lami maeneo yanayozunguka hifadhi ya serengeti ni wajibu wa serikali ili kuhakikisha mikoa yote inaunganishwa kwa barabara ya lami. Sehemu ya barabara hiyo itakayopita kwenye hifadhi ya serengeti, halitajengwa kwa kiwango cha lami, kama walivyoshauri wana mazingira.

Alionya wanaopotosha jitihada hizo za serikali hawaitakii Serengeti mema.

Kuhusu suala la migogoro baina ya wakulima na wafugaji, Mheshimiwa Kikwete alisema serikali ya CCM itahakikisha suluhu inapatikana. Jitihada zimeshaanza na anaamini hivi karibuni jawabu la kudumu la migogoro ya ardhi litapatikana

"Tumeagiza ardhi ya kila kijiji ipimwe, igawanywe na hati zitolewe kwa kila kijiji. Hadi sasa vijiji 37 vimeshaanza mpango huu". Alisema Mheshimiwa Kikwete.

Baada ya Mkutano huo wa Loliondo, Mheshimiwa Kikwete na msafara wake ulielekea Mugumu kwa mkutano mwingine wa kampeni.

No comments:

Post a Comment