9/17/2010

Mkutano wa Kampeni Monduli: Tobiko Kikwete Tobiko

Mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Jakaya Kikwete, akimnadi mgombea ubunge jimbo la Monduli mkoani Arusha, Edward Lowasa, kwa wapiga kura wa jimbo hilo wakati wa mkutano wa kampenni jana jioni.

Mgombea urais wa tanzania kupitia CCM, Jakaya Kikwete, akihutubia wananchi wa jimbo la Monduli mkoani Arusha jana jioni.
Wananchi wa jimbo la Monduli mkoani Arusha, wakinyanyua mikono juu kuonyesha kumuunga mkono mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Jakaya Kikwete, wakati akihutubia mkutano wa kampeni jimboni humo jana


Na Mgaya Kingoba, Monduli

“TOBIKO Kikwete, Tobiko,” yalikuwa ni maneno yaliyotamkwa na maelfu ya wananchi wa mji wa Monduli mkoani Arusha jana.
Neno hilo la lugha ya Kimasai lenye maana ya juu; lilitamkwa mara nyingi na umati uliofurika kwenye Uwanja wa Polisi mjini hapa kumsikiliza Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Kikwete akiomba kura.
Wananchi hao walieleza kwamba mgombea huyo hakuwa na sababu ya kufika kwao kuomba kura kwani wameshakata shauri kuwa ndiye chaguo lao.
Mbunge wa Monduli anayewania tena kiti hicho kwa tiketi ya CCM, Edward Lowassa, alikuwa kinara katika kuwaongoza wananchi hao kueleza hisia za furaha kwa Rais Kikwete, hasa baada ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005/2010, kutekelezwa kwa asilimia 99 jimboni humo.

“Tobiko Kikwete, Tobiko…Wataweza? Watamuweza Kikwete,” yalikuwa maneno yaliyotamkwa na Lowassa na umati huo kujibu, “Tobiko Kikwete, Tobiko’ pamoja na ‘Hawataweza, Hawatamuweza.’
Akizungumza kabla ya kuanza kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu, alimpongeza Rais Kikwete kwa mafanikio makubwa ya serikali yake akieleza kuwa amefanya kazi kubwa kuliko marais wote waliomtangulia, kutokana na uongozi mahiri na makini.
Aliyataja mafanikio yaliyopatikana katika Ilani jimboni Monduli kuwa ni ujenzi wa shule za sekondari za kata na kwamba mwakani watakuwa na shule tatu za elimu ya juu kwa sababu sekondari za kata zimekamilika.
Lowassa ambaye kila alipofafanua mafanikio ya Ilani, aliuliza umati na kuhoji Shukrani kwa nani na kujibiwa, ‘Kwa Kikwete,’ alieleza jinsi serikali ilivyowajali na kuwapata misaada wakati wa ukame mwaka jana uliosababisha vifo vya mifugo na ukosefu wa chakula, lakini hakuna mwananchi aliyekufa.
Alieleza pia upatikanaji wa maji umeboreka ingawa kumebaki maeneo machache likiwamo la kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), lakini watapatiwa mkopo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ajili ya huduma ya maji pamoja na mradi wa Benki ya Dunia kwa vijiji kadhaa.
Lowassa anayetumia kaulimbiu ya ‘Tulifurahi Pamoja, Tulihuzunika Pamoja na Tutasonga Mbele Pamoja na Tutashinda,’ katika kuomba kura, alisema wanajiandaa kujenga kiwanda cha kisasa cha nyama mjini Makuyuni.
Akimnadi Lowassa, Rais Kikwete alisema, “huyu ni mtu anayewapenda sana, anawahangaikia sana, haya yote (mafanikio) yanayosemwa sasa yametokana na juhudi zake…hakuna mwakilishi mzuri kushinda Edward Ngoyai Lowassa.
Naye Lowassa pamoja na Diwani mteule wa Kata ya Monduli Mjini, Issack Joseph, walieleza kwamba Rais Kikwete alifika hapo kuwasalimia tu kwani Monduli wameshafanya uamuzi kwamba huyo ndiye rais wao.

No comments:

Post a Comment