9/25/2010

Manyinyi aiteka Musoma Mjini

Na Mgaya Kingoba, Musoma

MGOMBEA Ubunge kwa tiketi ya CCM Jimbo la Musoma Mjini, Mathayo Manyinyi ameahidi kutowaangusha wananchi wa jimbo hilo na kuwataka waachane na waigizaji na kumchagua tena baada ya kusimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.

Manyinyi alishangiliwa kwa nguvu na umati wa wakazi wa jimbo hilo kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi ya Mukendo katika mkutano wa kampeni uliohutubiwa na Mgombea Urais, Rais Jakaya Kikwete, wakati akifafanua utekelezaji wa Ilani.

Bila kusoma mahali popote, Manyinyi alifafanua kila sekta ilivyohudumiwa na Chama Cha Mapinduzi katika Ilani ya 2005-2010 na katika kuthibitisha kuwa maneno yake ni sahihi, umati uliohudhuria mkutano huo ulikuwa ukimwitikia kwa sauti ya juu kila alipotaja mafanikio yake.

“Mukendo lami…Nyasho lami…Majita Road…Bweri sekondari…Baruti sekondari,” alieleza mgombea huyo anayeomba kipindi cha pili bungeni.

Manyinyi aliyataja mafanikio mbalimbali katika sekta za elimu ukiwemo ujenzi wa shule nyingi za kata; ujenzi wa barabara nyingi za lami; ujenzi wa zahanati na vituo vya afya na upatikanaji wa maji isipokuwa yanahitaji kuchujwa.
 
“Mheshimiwa Mgombea Urais hapa utekelezaji wa Ilani umekwenda vizuri. Nimekuwa nikipita katika mikutano ya kampeni, nimeahidiwa kura zote ni zangu. Hapa zimenyooka kama rula,” alieleza Manyinyi.

“Sitawaangusha, msihangaike na waigizaji,” alisema Manyinyi baada ya kunadiwa na Rais Kikwete. Kwa upande wake, Rais Kikwete alimuelezea mgombea huyo kuwa ni mbunge makini, mfuatiliaji hodari na kwamba yuko sawasawa katika kazi yake.

No comments:

Post a Comment