Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili Bariadi Mjini kwa mkutano mkubwa wa kampeni na kulakiwa na maelfu ya wananchi wa Bariadi.
Baada ya kuwasili kwenye uwanja wa mkutano wa Sabasaba Bariadi Mjini mnamo majira ya saa 11, Mheshimiwa Kikwete alielezwa wananchi wa Bariadi wamekuwa wakimsubiri mgombea huyo wa CCM tangu saa tatu asubuhi.
Akisoma Mafanikio ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2005 - 2010, Mgombea Ubunge Jimbo la Bariadi Mheshimiwa Andrew Chenge alisema kwenye mafanikio mengi hapakosi changamoto. Changamoto mojawapo ni ile ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Bariadi hadi Lamadi, ili kuunganisha Mkoa wa Shinyanga na Mwanza.
Changamoto nyingine ni maji na usambazaji wa maji safi yaliyochujwa kwa ajili ya wananchi wa Bariadi. Alimsihi Mwenyekiti wa CCM kuwafikiria wananchi wa Bariadi pindi atakapopata Urais ili kuhakikisha maji safi yanapatikana.
Akimkaribisha Mheshimiwa Kikwete kuzungumza na wananchi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa alisema wananchi wa Bariadi wana hamu kubwa ya kumsikiliza. Na kuongeza wakulima wa mkoa wa Shinyanga wametuma salamu za shukrani kwa Mheshimiwa Kikwete kwa kuongeza shillingi 80 kwenye bei ya kila kilo ya pamba mwaka jana wakati wa janga la mtikisiko wa uchumi. Wakulima wa Shinyanga hawatamsahau kamwe, na wanatambua kwamba yeye ni kipenzi cha wakalima, hawatomuangusha.
Naye Mgombea wa CCM, Mheshimiwa Kikwete alianza kwa kuwapongeza wana Bariadi kwa Wilaya yao kuzaa wilaya nyingine na kuwa wilaya mbili. Alisema yote hayo ni kusogeza maendeleo karibu na watu.
Alielezea sababu kuu tatu za wanabariadi kuchagua CCM kwanza CCM ni chama makini, pili kimeongoza nchi vizuri na tatu CCM ni waaminifu, wakiahidi wanatimiza.
Mheshimiwa Kikwete alizungumzia ahadi zilizowekwa na CCM mwaka 2005 za kuendeleza na kudumisha amani nchini, upanuzi wa elimu ya sekondari, kusambaza maji safi na salama vijijini. Kwa upande wa barabara Mheshimiwa Kikwete alisema ujenzi wa barabara Maswa - Bariadi na Bariadi - Lamadi zitajengwa kwa kiwango cha lami.
Suala la maji Mheshimiwa Kikwete alisema amelisikia na atalishughulikia. "Hilo la maji niachieni, nawaahadi nitahangaika nalo" alimaliza Mheshimiwa Kikwete akishangiliwa na umati mkubwa wa watu.
No comments:
Post a Comment