9/25/2010

Mkutano wa Kampeni Bunda - Wasira: Utanunuaje Urais kwa 20,000/=

Na Mgaya Kingoba, Bunda



MGOMBEA Ubunge kwa tiketi ya CCM katika Jimbo la Bunda, Steven Wasira amewataka Watanzania wasifanye majaribio na kubahatisha katika kuchagua urais kwa sababu mamlaka hayo ni makubwa na yanastahili kukabidhiwa kwa mtu mwenye akili timamu na chama cha maana.

 
Aidha, amehoji kwa vipi Watanzania wanaweza kununua urais kwa Sh 20,000, akihusisha na kauli ya Mgombea Urais wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa aliyekaririwa akisema akishinda, atafuta ada katika shule nchini.

Kwa sasa, ada kwa shule za sekondari za kutwa za serikali ni Sh 20,000 wakati elimu ya msingi hakuna ada. Kwa elimu ya chuo kikuu, serikali inatoa mikopo.


Aizungumza kwenye mkutano wa kampeni mjini Bunda mbele ya Mgombea Urais kwa tiketi ya chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, Wasira alisema urais ni mamlaka makubwa ambayo Watanzania hawapaswi kuyafanyia majaribio.


“Mwisho nataka kutoa ushauri kwa watu wa Bunda, Mkoa wa Mara na kwa Watanzania wote. Kwa mujibu wa Katiba yetu, mamlaka ya kiongozi wa serikali huchaguliwa na wananchi. Rais ni mamlaka makubwa,” alisema.


“Ndiye anayetangaza vita, kwa hiyo usiende kubahatisha, wala msifanye mambo ya kubahatisha, kujaribu. Ni lazima mchague mtu mwenye akili timamu, anayetoka chama cha maana. Mwalimu Nyerere alisema rais anaweza kutoka chama chochote, lakini Rais bora atatoka CCM.”

Huku akishangiliwa na wananchi, mwanasiasa huyo ambaye pia ni maarufu kwa jina la Tyson, alisema Watanzania ifikapo Oktoba 31, mwaka huu, hawapaswi kuchagua rais wa kubahatisha, wa kudanganya na msema uongo.


“Mtu anasema atauza saruji kwa shilingi elfu tano…kiwanda anacho? Bei ya mafuta inapangwa duniani na ina uhusiano na mataifa mengine katika masuala ya uchumi, yeye atamudu vipi,” alihoji Wasira ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.


Akimnukuu tena Baba wa Taifa, Wasira alisema kiongozi huyo aliwahi kuhoji kwamba ukiona mtu mzima anasema uongo, kuna mambo mawili; kichwani kwake kuna tatizo au anawadanganya watu kwa sababu anawadharau.


Alisema ahadi hizo za uongo ni pamoja na ile ya kutoa elimu bure, akieleza kuwa kwa Tanzania elimu ya msingi ni bure, ya sekondari ni Sh 20,000 na kwa vyuo vikuu kuna mikopo inatolewa, na kutaka wanasiasa waseme ukweli.


“Unaweza kununua urais kwa shilingi elfu ishirini? Ni ukweli daima ambao utaijenga Tanzania. Yapo matatizo na tunajua hayatakwisha baada ya uchaguzi, kwa sababu tatizo moja linazaa jingine,” alifafanua Wasira.

“Matatizo hayawezi kwisha, tunachosema ni kwamba tutaweza kuondoa vikwazo ili watanzania waende kasi katika kupata huduma za jamii na kujiletee maendeleo,” alisema Wasira ambaye wakati wote akieleza hayo, Rais Kikwete alikuwa akimfuatilia kwa makini na kumshangilia.


Akizidi kupiga vijembe kwa wapinzani, Wasira alisema katika harusi zote kuna wasindikizaji, na kuwataka wananchi wa Bunda kumwamini tena na kumpa ubunge, kuchagua madiwani wa CCM na kumrejesha Ikulu Rais Kikwete.
 
Akimnadi Wasira, Rais Kikwete alisema ni mbunge mzuri, anayemwamini, mchapakazi hodari, anayejituma na anamsaidia akiwa Waziri.

Mbali ya mkutano wa kampeni mjini Bunda, Rais Kikwete alifanya mikutano Kibara (Mwibara); Mkunyu (Musoma Vijijini) na Musoma Mjini. Leo atafanya mikutano Magu mkoani Mwanza na Bariadi mkoani Shinyanga.

No comments:

Post a Comment