9/09/2010

Mkutano wa Kampeni Mkwakwani : JK - Tanga "Kuzaliwa" Upya

Na Mgaya Kingoba, Tanga
ULE wimbo wa Tanga Kunani, ulioimbwa na wasanii akina John Walker na Mkoloni,
muda si mrefu utabidi utungiwe sehemu ya pili kwani Serikali ya CCM imepania
kuubadili mji wa Tanga na kuwa wa viwanda.
Tanga ile ya zamani iliyokuwa ikifahamika enzi hizo kwa mashamba ya mkonge na
viwanda kadhaa vikiwamo vya chuma, mbolea, sabuni na katani, itazaliwa upya
katika miaka mitano ijayo.
Tayari eneo la Neema katika barabara iendayo Pangani kutoka Tanga, imetengwa kwa
ajili ya kutekeleza azma hiyo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya
2010 – 2015.
Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Kikwete ameueleza umma wa wakazi wa
Tanga na vitongoji vyake jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini hapa kuwa hilo
limo ndani ya Ilani hiyo na litatekelezwa.
“Tanga mji ambao ulijengeka juu ya mkonge, na ukafa baada ya mkonge kudodora,
sasa utazaliwa upya. Nia ya CCM katika miaka mitano ijayo ni kuufanya Tanga kuwa
mji wa viwanda,” alisema Rais Kikwete na kushangiliwa na maelfu ya wananchi
waliojitokeza kumsikiliza akiomba kura.
Alisema Tanga ulikuwa mji wa pili kwa ukubwa baada ya Dar es Salaam, sasa
utakuwa mji wa viwanda utakaojengwa katika eneo la Neema katika Barabara ya
Pangani na utakuwa kituo cha biashara.
Alisema katika kutekeleza hilo, ndiyo maana wanajenga bandari mpya eneo la
Mwambaji jijini hapa na pia watafufua reli ya Tanga – Arusha hadi Musoma, ambayo
itakuwa ikibeba bidhaa mbalimbali zikiwemo za kwenda Uganda.
Alisema bidhaa hizo za Uganda zitakuwa ni zile zinaingizwa na zinazotoka katika
nchi hiyo ambayo haina bandari.
“Kwa kuifanya Tanga kuwa mji wa viwanda, biashara itakuwa kubwa, na tutatoa
ajira nyingi. Kwa hiyo, tunataka kuifanya Tanga irejee katika hadhi yake,”
alisema Rais Kikwete.
Mbali ya hayo, alielezea utekelezaji wa Ilani iliyopita ikiwemo kujengwa kwa
barabara za Mkoa wa Tanga; huku akiahidi kuboreshwa kwa upatikanaji wa umeme na
maji, na tayari zimetengwa Sh milioni 261 kwa ajili ya kupata maji.
Kuhusu afya, alisisitiza uboreshaji wa hospitali, zahanati na vituo vya afya,
lakini akawaonya wananchi wa Tanga kuhusu idadi kubwa ya maambukizi ya ugonjwa
wa Ukimwi ambayo ni asilimia 9.7.
Akimnadi mgombea ubunge, Omar Nundu, Rais Kikwete alisema ni msomi aliyebobea,
mwenye taaluma ya uhandisi katika masuala ya anga; anayemuunga mkono na
atawasaidia sana wananchi wa Jimbo la Tanga.
Kwa upande wake, Nundu alisema atashirikiana na serikali kuleta maendeleo kwa
wakazi wa Tanga, lakini alifunika zaidi mkutano huo, alipotumia neno la Kidigo,
‘Zindama’ kumtambulisha Rais Kikwete na mwitikio wake ulikuwa mkubwa, kiasi cha
kumfanya Rais naye ajiunge katika kumnadi kwa kibwagizo hicho chenye maana ya
juu.
Mgombea huyo wa CCM anaanza mapumziko ya siku tatu leo kupisha sikukuuu ya Idd
el Fitr, kabla ya kuendelea na kampeni.

No comments:

Post a Comment