9/21/2010

Mikutano ya Kampeni Iringa: Ilula, Isimani, Kalenga, Kilolo





Na Mgaya Kingoba, Iringa
MGOMBEA wa Urais kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Kikwete ameahidi kuwa serikali ya chama hicho itaongeza mara tatu idadi ya wananchi wanaonufaika na ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa mfumo wa vocha.
Aidha, amewataka wananchi wa Mkoa wa Iringa kutojirahisisha na kujisahau katika suala la ugonjwa wa Ukimwi, kwani kasi ya maambukizi inatisha.
Rais Kikwete aliyasema hayo kwa nyakati tofauti alipohutubia mikutano ya kampeni za Uchaguzi Mkuu leo katika majimbo manne ya Mkoa wa Iringa ya Kilolo; Isimani; Kalenga na Iringa Mjini akiomba kura kwa wananchi hao.
Akizungumzia ruzuku za pembejeo za kilimo, alisema kwa sasa serikali inatoa ruzuku ya pembejeo kwa mfumo wa vocha kwa wakulima milioni mbili na kwamba katika miaka mitano ijayo, itafikisha wakulima milioni sita.
“Yamekuwepo mafanikio makubwa katika utumiaji wa pembejeo za kilimo na tumeongeza fedha na idadi ya wakulima tangu tuingie madarakani. Kwa sasa, wakulima milioni mbili wananufaika, tutaongeza idadi kufikia milioni sita katika miaka michache ijayo,” alisema Rais Kikwete.
Akiwa Ilula jimboni Kilolo, mbali ya kueleza mafanikio ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM, alieleza kwamba Ukimwi ni tatizo kubwa katika mkoa huo kwa sababu ndio unaoongoza kwa idadi ya maambukizi ukiwa na asilimia 15.
Alisema hiyo ni mara 10 ya wastani wa Kitaifa ambao ni asilimia 5.8, na ndiyo maana aliagiza kuwapo kwa mpango maalumu kwa mikoa ya Iringa na Mbeya kuona kwa nini kiwango chao cha maambukizi kiko juu.
“Lakini ugonjwa wa Ukimwi ni wa kujitakia. Unaweza kuamua kutopata Ukimwi, kwani
ile njia inayoleta Ukimwi, mwanadamu hana dharura nayo. Tafadhalini sana, tuache
kujirahisha, tusijisahau,” alieleza Rais Kikwete.
Akiwa katika Jimbo la Isimani, alieleza alikubali kubeba jukumu la kuhakikisha Isimani inapata maji ya uhakika ambako kwa mujibu wa Mbunge Mteule wa jimbo hilo, William Lukuvi, kuna mradi wa maji unaohitaji Sh bilioni tano.
Lukuvi alisema mradi huo ukikamilika, utaviwezesha vijiji 30 vya Jimbo la Isimani kupata maji ya uhakika, na hivyo kumaliza tatizo hilo.
Kwenye Jimbo la Kalenga, alieleza kuwa sasa serikali yake inaelekeza macho katika kuiwekea lami barabara inayokwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ambayo ndiyo hifadhi kubwa kuliko zote Tanzania.
Katika mikutano yake yote ya jana ambayo alitumia helikopta kufika mahali ikopangiwa kuhutubia, aliwanadi wagombea udiwani na ubunge ambao ni Profesa
Peter Msolla (Kilolo); Lukuvi aliyepita bila kupingwa Isimani; Dk. William
Mgimwa (Kalenga) na Monica Mbega (Iringa Mjini).

No comments:

Post a Comment