9/23/2010

Mkutano wa Kampeni Mbarali, Mbeya: Obama aipa chapuo Tanzania

Na Mgaya Kingoba, Mbarali

MAREKANI imesema kwamba Tanzania ni moja ya nchi inazozipigia mfano miongoni mwa nchi zinazoendelea, kwa uongozi bora na unaodumisha utawala bora na utawala wa
sheria.

Kwa mujibu wa Rais Jakaya Kikwete, Rais Barack Obama wa Marekani aliyasema hayo jana wakati akihutubia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York, nchini humo.

Rais Kikwete alisema wakati akihutubia mkutano mkubwa wa kampeni kwenye Uwanja wa Barafu mjini Rujewa wilayani hapa katika Mkoa wa Mbeya, kuomba kura kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Alisema muda mfupi kabla ya kuhutubia maelfu ya wananchi uwanjani hapo, alizungumza na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Leonhadt, na kumuelezea jinsi Rais Obama alivyoimwagia sifa Tanzania katika hotuba yake UN.

“Kabla ya kupanda hapa jukwaani kuzungumza nanyi, mliniona nazungumza na simu…alikuwa Balozi wa Marekani, ananiuliza kama nimesikia hotuba ya Rais Obama jana usiku kwenye Umoja wa Mataifa,” alisema Rais Kikwete.

“Nikamwambia niko huku nahangaika, nitasikia saa ngapi? Wakati mwingine niko hoi bin taaban hata kusikiliza redio au televisheni huna muda.

“Ameniambia kuwa Rais Obama ameeleza misingi ya Marekani kusaidia nchi zinazoendelea, na mfano wake akatoa Tanzania. Akasema nchi yetu inaongoza kwa kujali utawala bora, utawala wa sheria, kuheshimu NGO,s, na tunatawala vizuri,” Rais Kikwete aliwaeleza wananchi.

“Kama siyo mimi na akina Mwandosya, nani mwingine anayemsifu,” alisema Rais Kikwete akimtaja Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya, ambaye alikuwapo kwenye mkutano huo akiwa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) kupitia Mkoa wa Mbeya.

Alisema kauli hizo za Marekani kuisifu Tanzania, hazitoi yeye, lakini kila anapofanya hivyo, baadhi ya watu huhoji kwani kila mara na Marekani.

“Nikisema sifa hizi zinazotolewa na Marekani, watu wanasema, ‘huyu naye na Marekani kila siku.’ Wanasema wenyewe, siyo mimi,” alifafanua Rais Kikwete.

Marekani imekuwa mshirika mkubwa wa maendeleo kwa Tanzania tangu Rais Kikwete aingie madarakani miaka mitano iliyopita, ikitoa ufadhili mkubwa katika miradi mbalimbali ya sekta za elimu, afya, miundombinu na nishati.

Chini ya Shirika la Milllennium Challenge (MCC), Marekani itafadhili miradi ya umeme katika mikoa sita nchini; itajenga barabara kadhaa ikiwemo ya Tunduma-Laela- Sumbawanga na hivi karibuni ilitoa vitabu 800,000 kwa ajili ya shule za sekondari nchini hasa kwa masomo ya sayansi.

No comments:

Post a Comment