9/28/2010

Mkutano wa Kampeni Kahama Mjini: Wakazi wa Kahama wampa asante JK

Wakazi wa Kahama wamempa asante Mheshimiwa Jakaya Kikwete kwa kutekelezewa ahadi mbili kuu ambazo aliziweka na kuahidi kuzitekeleza kwa wakati.

Ahadi hizo ni ile ya kuupa hadhi mji wa Kahama ambapo tarehe 1-07-2010 Kahama iliwekwa rasmi kuwa Halmashauri ya Mji na ile ya kusambaza maji mji wa Kahama na kufanya idadi ya wakazi wanaopata maji mjini hapa kuongezeka zaidi ya mara kumi.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa amemsihi Mwenyekiti wa CCM taifa Mheshimiwa Kikwete kukamilisha ujenzi wa barabara itakayojengwa kwa kiwango cha lami ambayo tathmini yake imekamilika na tayari imekwisha anza kujengwa.

Akizungumza na wananchi wa Kahama, naye Mheshimiwa Kikwete alifafanua mafanikio hayo ya CCM kwenye ahadi kuu zilizoorodheshwa kwenye ilani ya CCM ya 2005.

Akizungumzia ahadi ya kusambaza maji Mheshimiwa Kikwete alisema vijiji 15 vilivyopitiwa na bomba kuu la maji kutoka Ziwa Victoria, vitaletewa maji kwenye kila kaya. Fedha zimeshatengwa ili kuhakikisha ahadi hiyo inafanikiwa.

Huduma ya umeme nayo ilizungumziwa ambapo vijiji 11 vya Kahama vitapata umeme kutokana na mradi mkubwa wa serikali wa kusambaza umeme. Umeme huo utapita kuelekea Ushirombo ambapo pana tatizo la upatikanaji wa umeme.

Kwa upande wa kilimo, Mheshimiwa Kikwete alisema aliahidi 2005 kwamba CCM itafanya mageuzi ya kilimo chini. Leo miaka mitano baadaye, safari hiyo imeanza ambapo hatua saba muhimu zimechukuliwa ili kuhakikisha wakulima wa Tanzania wanafaidika na shughuli ya kilimo.

Hatua hizo ni ujenzi wa barabara ili bidhaa za kilimo zipite kwenda sokoni, usambazaji wa ruzuku ya mbegu, mbolea, dawa za mimea, utafutaji wa masoko, upatikanaji wa maji na upatikanaji wa pembejeo za kilimo.

Kwa upande wa barabara, Mheshimiwa Kikwete alisema hata yeye anakubaliana na kilio cha wakazi wa Kahama wa kujengewa barabara yao. Alisema fedha ipo na haoni sababu ya ujenzi wa barabara hiyo kusimamishwa. Alimalizia huku umati mkubwa wa watu ukimshangilia alipotaja juu ya ujenzi wa barabara hiyo.

Mwisho aliwanadi wagombea wa udiwani na ubunge wa CCM na kuwasihi wana Kahama kuchagua CCM

No comments:

Post a Comment