9/13/2010

Bumbuli yafunika mapokezi ya Mheshimiwa Kikwete


Maelfu ya wakazi wa jimbo la Bumbuli wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga wakimshangilia mgombea urais kupitia CCM, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete mara alipowasili kwenye mkutano mkubwa wa kampeni.

Msafara wa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete umepokelewa kwa shangwe na umati mkubwa wa watu na wapenzi wa CCM Bumbuli wilani Lushoto jioni hii.

Msafara huo uliowasili eneo hilo mnamo saa kumi na moja jioni, ulilakiwa na maelfu ya wananchi walioonekana kwenye vilima vyote vya uwanja wa mkutano wa Togotwe, Bumbuli.

Kabla ya kumtambulisha Mwenyekiti wa CCM Taifa, Katibu wa CCM wilaya alimkaribisha Katibu Mkuu wa CCM Mheshimiwa Luteni Mstaafu Yusufu Makamba aliukaribisha rasmi msafara huo ambapo aliwaambia wana Bumbuli wachague chama bora, chama safi CCM pamoja na wagombea wake kwa nafasi ya urais, ubunge na madiwani.

Naye Mgombea urais Mheshimiwa Kikwete akizungumza na umati huo, alikiri kuwa Bumbuli imetisha kwa mapokezi makubwa na jinsi wananchi wa hapo walivyoikubali CCM na wagombea wake.

Akinadi sera za CCM, Mgombea Urais CCM Mheshimiwa Kikwete alisema tatizo sugu la maji litashughulikiwa hivi karibuni na vijiji kumi na nne vya jimbo hilo vimepewa kipaumbele kwenye mradi huo mkubwa wa maji. Pia Mheshimiwa Kikwete aliahidi barabara ya kiwango cha lami itajengwa kama ilivyoahidiwa kwenye ilani ya CCM 2010-2015 kupitia Bumbuli, Dindili, Soni hadi Karogwe.

Akiwanadi wagombea wa Bumbuli, Mheshimiwa Kikwete aliwashukuru wananchi wa Bumbuli kwa kumpitisha January Makamba bila kupingwa. Alimsifu akisema kuwa ni kijana mzuri, mwenye akili sana, alikuwa msaidizi wake yeye binafsi alipokuwa Wizara ya Mambo ya Nje na hata Ikulu.

Naye mgombea Ubunge Jimbo la Bumbuli, January Makamba, alimshukuru Mheshimiwa Kikwete kwa kumuamini, kumlea kisiasa wakati akiwa msaidizi wake kwa miaka yote. Aliahidi kuwa CCM itapata kura za kishindo kutokea Jimbo la Bumbuli. Pia alichukua nafasi hiyo kuomba Jimbo la Bumbuli kuwa wilaya kwani linakidhi vigezo vitano kati ya vinane vya kuwa wilaya.

2 comments:

  1. Kikwete na January mnakubalika sana Bumbuli, mtashinda kwa kishindo, lakini jamani msije mkajisahau hasa katika utekelezaji kwa vitendo suala la kilimo kwanza, kwani eneo hili ustawi wake unategemea sana kilimo hasa cha matunda na mbogamboga. Hasa wewe January, maana una added advantage ya kuwa karibu na Rais!

    ReplyDelete
  2. JK & JM

    Barabara! Kampeni ya kisayansi yenye ufanisi iendelee pasi kukoma hata baada ya uchaguzi.

    Nawatakieni baraka & kila la kila la kheri hadi ushindi.

    ReplyDelete